Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kupata nafasi. Pia, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii siku hii ya leo ya kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na kuweza kusema machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninapenda kutoa pole kwa wananchi wangu wa Jimbo la Bunda Mjini na Watanzania kwa ujumla ambapo tumempoteza aliyekuwa Mkurugenzi wa TANESCO ndugu yangu Gesima Nyamhanga ambaye ni mzawa jimboni kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la msiba huu wa ndugu yetu Gesima Nyamhanga tumelipokea kwa masikitiko makubwa na wananchi wangu wa Jimbo la Bunda Mjini, lakini hatuna namna, yote haya ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Ninawaomba tu wawe watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu mpaka pale ambapo tutapata nafasi ya kuweza kumsitiri katika nyumba yake ya milele na tumwombee heri kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumpokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kuhakikisha kwamba Jimbo letu la Bunda Mjini linapata miradi mbalimbali ya maendeleo na kuufanya Mji wetu wa Bunda uweze kupata mabadiliko makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata miradi mingi katika kipindi hiki cha miaka minne ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali yetu ya Wilaya ya Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Bunda ikiwa ni pamoja na kituo cha Afya katika Kata ya Waliku, kujenga zahanati katika kata zetu, kuimarisha miundombinu ya maji katika kata zilizoko pembezoni mwa Mji wa Bunda, kuhakikisha umeme unapatikana katika maeneo yote ya vitongoji katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa miaka minne/mitano iliyopita Halmashauri ya Mji wa Bunda barabara zile za mitaa zilikuwa haziwezi kupitika na ziko ndani ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, lakini kwa kipindi chake hiki cha miaka minne tumepata barabara nyingi na barabara zote sasa zinapitika. Tumefungua barabara mpya nyingi ambazo zinaifanya Halmashauri ya Mji wa Bunda ipitike kila mahali unakoweza kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata pia vyumba vya madarasa, shule za sekondari vyumba vya kutosha. Vinawafanya wanafunzi wetu waweze kupata elimu iliyo bora kwa sababu mazingira yametengenezwa vizuri. Tumepata shule ya awali ya ufundi ambayo inajengwa kwenye Kata ya Sazira ambapo sasa iko kwenye hatua za mwisho ili iweze kuchukua wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri ya Mji wa Bunda tuko kwenye miradi ile ya TACTIC ya Miji 28 ambayo inakuja kuboresha miji na kuufanya Mji wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kuwa mji wa kisasa na mradi huo ndiyo mradi ambao wananchi wetu wa Jimbo la Bunda Mjini wanausubiri kwa hamu kubwa na matarajio makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa sababu mchakato wa kwanza ambao utakwenda kujenga stendi, soko na lami kilometa 25.3 kwenye Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda umeanza. Kwa hiyo, itaifanya Halmashauri ya Mji wa Bunda kuwa kivutio na kwa sababu iko pembezoni ya Mbuga ya Serengeti na ndiyo sehemu na lango la kuingilia Mkoa wa Mara inaufanya mji ule uweze kuvutia na kuwafanya wawekezaji waweze kuongezeka katika Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya wawekezaji vipo vya kutosha ambavyo vimepimwa na halmashauri. Kwa hiyo, watu wote ambao wanajihisi kwamba wanaweza kuwekeza Bunda tunawakaribisha kwa sababu maeneo yapo ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya na kwa namna ambavyo amesimamia miradi mikubwa ya Serikali kwa miaka hii mitano na kuhakikisha kwamba miradi mingi imetekelezeka vizuri. Kwa kweli tunamshukuru kwa sababu amekuwa ni msimamizi mahiri ambaye pia ameifanya Serikali imeweza kutekeleza miradi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nchi yetu ina tatizo la ajira kwa wananchi wake, lakini mimi ni mfanyabiashara kwa zaidi ya miaka 25. Miaka 25 iliyopita tuliokuwa tukianzisha biashara na zama hizi za leo za mwaka 2025 ni zama tofauti. Miaka 25 iliyopita ilikuwa kijana wako anaweza akamaliza shule ukampa mtaji wa shilingi milioni moja au milioni mbili akaenda mtaani akafanya biashara na akapata matokeo, lakini leo kitu hicho hakiwezekani. Hakiwezekani kwa sababu ya mambo mbalimbali na gharama mbalimbali za uendeshaji wa kibiashara ambazo zimejitokeza na ambazo zinawakabili wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninafikiri kwamba ni vizuri Serikali itengeneze mpango maalum kuhakikisha kwamba inatengeneza uwiano wa kodi kwa wafanyabiashara. Wafanyabiashara wanaweza kulipa kodi, lakini pia wafanyabiashara wanahitaji kuelimishwa zaidi ili waweze kulipa kodi kwa hiari yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, saa nyingine huwa najiuliza kwamba bajeti ya Serikali labda ni shilingi trilioni 30 inayokusanywa kutoka kwa wafanyabiashara, hii shilingi trilioni 30 inayokusanywa kutoka kwa wafanyabiashara inajulikana inakusanywa kutoka kwa mfanyabiashara gani na kwa kiasi gan?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni hivyo ni kwa nini tufikie mahali ambapo labda viongozi wa Serikali wanaweza kwenda kuvutana na wafanyabiashara kwa sababu ukimwelimisha vizuri mfanyabiashara akaelewa suala la kulipa kodi ni suala la hiari na lazima ataenda kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi nikasema Serikali ni vizuri itengeneze miundombinu mizuri kati yake na wafanyabiashara ili wafanyabiashara hawa waendelee kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao. Leo hii vijana wetu wakipewa mitaji hii ambayo Serikali imefanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba inatoa hela kwenye halmashauri halafu fedha zile yanakopeshwa makundi maalum yakiwemo ya vijana, lakini leo kijana akipata mtaji wa shilingi milioni moja akaenda nao sokoni, saa nyingine mtaji huo utaishia kwenye gharama za uendeshaji kabla ya kufungua biashara yake. Atalipa kodi na michango mbalimbali kabla ya kufungua biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huko masoko yetu ya biashara yameingiliwa na watu wengi ikiwa ni pamoja na wageni wa kutoka nje ambao wao wakija kwenye nchi yetu na mitaji yao inakuwa ni mitaji mikubwa kuliko mitaji yetu sisi Watanzania, kwa sababu fedha zetu zinakuwa kwenye thamani ya chini na fedha zao zinakuwa na thamani ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapowapeleka watu wetu katika ushindani wa kibiashara na hawa watu hawataweza ku-compete kwa sababu wale wataonekana wanaweza kufanya biashara kubwa kuliko watu wetu. Zaidi ya hapo tutakuwa na vijana ambao watakuwa wapo na wanapata mitaji hii ambayo wanakopeshwa na Serikali wanaitumia na hawawezi kurejesha kwa sababu ya miundombinu ambayo imetengenezwa. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ifanye kila linalowezekana kuwalinda wafanyabiashara wake wadogo walioko nchini, kwa kutengenezea njia madhubuti ambayo itawafanya waweze kufanya biashara zao kwa uhuru, lakini kulingana pia na mitaji yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu ana mtaji wake huu wa shilingi milioni moja au milioni mbili akapelekewa kodi ya shilingi 800,000 katika mtaji wa shilingi 2,000,000 haitawezekana kulipa hiyo kodi, kwa vyovyote vile atakukwepa tu, lakini ukitengeneza miundombinu ambayo itamfanya katika shilingi milioni mbili aliyonayo akaona kodi ni chini ya shilingi 200,000 anaweza kulipa vizuri, nje ya hapo utalaumiana na wafanyabiashara na mwisho watakwepa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba Watanzania hawataki kulipa kodi, wanataka kulipa. Pia, tunataka wale ambao wanasimamia kwenye vitengo vya kodi na wao wasaidie kujua wafanyabiashara namna ya kulipa kodi katika usawa ambao unawaruhusu kuishi katika maisha yao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)