Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunichagua kuchangia katika hii hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetujalia sote tuwe hapa tukiwa na afya njema. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Makamu wa Rais; na Mawaziri wote ambao Mwenyezi Mungu amewapa nafasi hii ya kuweza kukaa na kusimamia mambo mbalimbali ya kiutendaji na kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazidi kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kuitanguliza nchi yangu ambayo iko katika amani na utulivu. Mheshimiwa Rais amesimamia amani na utulivu, bila amani na utulivu hakuna biashara, hakuna kilimo, hakuna uchimbaji wa madini. Unaweza ukawa na rasilimali, lakini nchi yako kama haina amani, utulivu na utu ndani yake hakuna kazi. Katika kipindi alichopewa Mheshimiwa Rais ameweza kusimamia vitu hivyo vyote. Mwenyezi Mungu amlinde na amwezeshe na kumwongezea ili anakokwenda Mwenyezi Mungu azidi kumwongezea afya njema. Hii siyo amri yake ni kadari ya Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kumpa utu na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka katika Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na nitazungumzia suala la watu wenye ulemavu. Kutokana na statistics ya mwaka 2023 tuna walemavu milioni 10.7 hili ni kundi kubwa sana na hili kundi linakwenda katika mambo mengi iwe maendeleo ya kilimo, uchumi mpaka siasa wao wanatakiwa wawemo katika maeneo hayo. Nitazungumzia fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu, nilisikia mwenzangu Mheshimiwa Ikupa pale hizi fedha wamepewa hizi walemavu ziwasaidie katika vyama vya walemavu kuwasaidia kununua vifaa tiba na vifaa saidizi. Zile fedha hazikuletwa kwa ajili ya economic recovery, hapana! Zile 4:4:2 msichanganye na hizi pesa kwa nini? Hamjajua maumivu na machungu wanayopitia watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nenda Ocean Road walemavu wana kansa za ngozi. Mafuta yanayonunuliwa haya ndiyo yanakwenda kusaidia haya makundi maalum. Leo unapoitoa ile hela unaipeleka sehemu nyingine wale watasaidiwa na nani? Je, waendelee kuteseka na ngozi wakati hela zilikuwepo? Tunazungumza leo huu mwezi Aprili, hela imetengwa toka mwezi Julai mpaka leo haijatoka hata senti tano. Ninaamini sana Waziri yupo vizuri, Katibu Mkuu yupo vizuri, asimame na watendaji wake. Tunazihitaji hizi bilioni zirudi zikanunue dawa tuokoe maisha ya watu wenye ulemavu ambao wanayahitaji haya mafuta na baadhi ya vifaa saidizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana mimi mwenyewe unaniona ninahangaika kutafuta kila mahali kugawa wheelchair kila mahali, kwa nini? Hawa watu wanahitaji kuokolewa. Chukueni mfano akinamama anabeba mtoto mwenye matatizo, mtoto huyo anambeba mpaka mtoto ana miaka 20 yupo mgongoni, lakini ukimpa wheelchair umemwokoa mwanamke, umeokoa mazingira magumu anayopambana nayo mwanamke anayetafuta chakula anatafuta biashara, lakini hawezi ana mtoto mlemavu mgongoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba kwa uchungu niliokuwa nao tuwe wote humu ndani tuuangalie huu uchungu hizi pesa zirudi na siyo zirudi watuambie hapa baada ya hotuba hii ya Waziri Mkuu, lini watazirudisha hizi hela zikafanye kazi? Tayari hela zilishatengwa hela za vijana. Zilitengwa hela za vijana shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya mafunzo yao na maendeleo yao. Mpaka leo tunazungumza hata senti tano. Ninazungumza kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati, hazijaingia. Leo kijana anahitaji kujitegemea, watu wanamaliza vyuoni hawana ajira hela hizi ndiyo wanaweza kusaidiana kwa mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea Tengeru - Arusha, vijana ni ma-graduate wanalima mboga, lakini je, kama hawana pesa yao ya ruzuku tunafanya nini? Tusitumie nguvu na mabavu kuwanyang’anya hawa vijana hela zao, tunaomba hizi pesa ziende kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishukuru sana Bunge lako Tukufu likiongozwa na Mheshimiwa Spika amelifanya Bunge limekuwa la utulivu sana na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tupo hapa utulivu huu na amani hii inateremka mpaka chini na ni imani yangu kuwa katika uchaguzi tunaokwenda nao na tulivyofikia hapa Mungu atatufikisha katika utulivu na amani hakuna kumwaga damu. Dunia yote inaiangalia Tanzania kwa mifumo na mazingira mazuri tuliyoyaweka kwa ajili ya utulivu na Mwenyezi Mungu atasimama na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukurani sana kwa Mheshimiwa Rais, Waziri wa Kilimo, kwa mara ya kwanza mazao ya kilimo hasa korosho, ufuta na mbaazi zimeruka kwa bei ambayo wananchi sasa hivi kila unayemuuliza yupo mashambani wanalima. Korosho ya kwanza grade one imeuzwa kwa shilingi 4,000 kutoka shilingi 1200; namba mbili, imeuzwa kwa shilingi 3,800; namba tatu shilingi 3,500, haya ni mabadiliko makubwa. Ufuta umeuzwa mpaka shilingi 4,000, mbaazi ambayo ilikuwa inauzwa shilingi 100 sasa hivi mbaazi inakwenda mpaka shilingi 2,500 hatuna cha kusema zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba niyashukuru mashirika mbalimbali ambayo yameonesha upendo wa kufanya value addition kwa vijana. Mamlaka ya Korosho wanagawa au wanasaidia vijana mashine za kubangua korosho. Hii maana yake itawakwamua vijana kujiajiri wenyewe badala ya kuombaomba mtaani. Hii ni value addition ambayo tunaitaka. Unaposikia hao Wachina au watu wa India waliendelea waliwasimamia vijana kwa biashara ndogondogo. Leo ukimpa kifaa cha kubangua korosho atabangua atafanya packaging mafunzo atakwenda na yeye mwenyewe ataweza kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimetolewa mashine vilevile kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Leo mlemavu asiyeona, lakini ana mke na watoto ukimpa mke wake ataweza kubangua korosho yule mke wake na watoto wake wataweza kujikwamua kiuchumi na kuweza kujiendeleza katika uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais wameweza kugawa maeneo Mbogwe, Kahama. Leo walemavu na viziwi wanachimba dhahabu Kahama kitu ambacho ni mafanikio makubwa ambayo hatukutegemea mtu ambaye ni mlemavu akaweza kuchimba dhahabu. Mwenyezi Mungu awajalie na tumshukuru vilevile Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO ametoa mitambo mikubwa ya kwenda kuchimba dhahabu kule Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo; hapa ninapozungumza kuna vikundi vya vijana wenye ulemavu wa ngozi wamepewa mashamba Hombolo na hapa Bihawana na tayari wanalima alizeti. Ninasema hakuna kuachwa nyuma katika maendeleo. Katika maendeleo ukisema unakwenda na hawa, ukawaacha walemavu ina maana hujawatendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika siasa tuna asilimia tatu ya watu wenye ulemavu ambao wanatakiwa waingie ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, apitie kokote, lakini anayo haki ya kimsingi, lakini mpaka sasa hivi tuna Wabunge walemavu ambao wameingia ni watatu tunahitaji nafasi tisa extra ziingie hapa kwa ajili ya kundi maalum, hii ni Sheria ya Umoja wa Mataifa. Kama nchi hii iliridhia watu wenye ulemavu wana haki ya kuingia katika Bunge hili kwa asilimia yao. Nina imani kuwa Serikali tukufu na sikivi italisimamia hili, itaendana nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mifuko ya Jamii; Waheshimiwa Wabunge tumetembelea Mifuko yetu ya NSSF, PSSSF, OSHA, WCF na CMA. Cha kusema sina, tulikwenda kwanza NSSF ilikuwa inakufa na ilishakufa. Leo NSSF katika mradi mmoja ule tu kwanza wa Kigamboni umeweza kupunguza matatizo mengi na kufanya ule Mfuko uweze kujiendesha. Niliomba Daraja la Busisi tuipatie NSSF, kwanza wana uzoefu katika uzoefu huu utailetea uchumi na itaweza kuifanya NSSF ambayo ilikuwa inaanguka kuweza kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu PSSSF; tulitembelea PSSSF tukaona maendeleo makubwa na uchumi. Zamani tulikuwa tunagemea hii Mifuko ambayo waliiwekeza katika maeneo ambayo yalikuwa hayazalisha tutafanyaje watu watakapokuwa wanastaafu? Kwa kweli Mifuko yote inafanya kazi vizuri. Sasa hivi tuna imani hata kama mtu anastaafu hatazungushwa tena kwanza tuna kwenda kidigiti na wanafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu OSHA; mwanamke jembe anaitwa Khadija Mwenda amefanya kazi. Kwa kweli mimi mwenyewe nikimwona mwenyewe nina-relax hapa mbele sina cha kufanya ni kumwachia mwanamke mwenye uwezo aendelee. WCF, kwa kweli Mifuko hii yote inafanya kazi vizuri. Wamechaguliwa watu ambao ni wasikivu wanasimamia na tunazidi kuwaombea angalau wasiachwe ili angalau miaka mitano hii wazidi kuboresha katika maeneo haya ili tuweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia bandari, katika njia kuu nne za uchumi mojawapo ni bandari, barabara, anga na mawasiliano. Bandari ambayo tulitegemea itakufa, lakini inakwenda vizuri sana. Ombi langu Serikali yangu isimamie bandari zile ndogondogo 56 ziende ikiwepo Bandari ya Lindi. Bandari ya Lindi na Mtwara sasa hivi itakuwa ni uchumi mkubwa wa kuunganisha Comoro na Tanzania na tayari wameshaingia katika mikataba ya kuhakikisha Comoro watatumia Bandari ya Lindi na Bandari ya Mtwara kuchukua mizigo yao ya kupeleka kule Comoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ilikuwa ni barabara, Mheshimiwa Rais baada ya kuiona barabara ya Lindi imefikia kiwango kile ametoa shilingi bilioni 600 ya kuanza nayo kwenye ile Bandari ya Lindi, Barabara ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara, lakini inavuka mpaka Mozambique na inavuka mpaka South Africa, watu wote wanatumia bandari hii, kwanza ni karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kitendo cha Mheshimiwa Rais cha kutoa hizo pesa tunasema Mwenyezi Mungu azidi kusimama. Ombi langu wakandarasi wasije wakatuangusha. Kutolewa pesa kwa wakati na wao wafanye kazi yenye ubora ili angalau haya tunayoyakusudia maendeleo ya kiuchumi ambayo yataunganisha Tanzania, Mozambique mpaka South Africa iweze kufanyika kazi na sisi hatuna cha kusema. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu aijalie Bandari ya Lindi na tayari tumeshatengenezewa fungu la kuweza kurekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Lindi, bidhaa badala ya kutoka mikoa ya mbali zitakuwa zinatoka Lindi kwenda Comoro. Lindi na Comoro ni kama unavyozungumzia Dar es Salaam na Zanzibar. Hivyo, tukisema biashara hii tuiendeleze itakuwa tumefanya jambo zuri sana na kazi nzuri sana ya Balozi wetu Yakubu ambaye yuko Comoro ya kusimamia, kuhakikisha bandari hizi za Lindi na Mtwara zinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Mtwara ni one of the best bandari ambayo itabidi tuifanyie kazi. Bandari ya Mtwara kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam na kutoka Zambia kwenda Mtwara, ni karibu kwenda Mtwara kuliko kwenda Dar es Salaam. Kutoka Malawi kwenda Mtwara ni karibu kuliko kuja Dar es Salaam. Tukizidi kuisimamia ile Bandari ya Mtwara tutazidi kusimamia uchumi ambao utaweza kufanya mikoa hii iweze kupata ajira na kuondokana na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, habari yangu ya mjusi naingojea Wizara ya Maliasili nitaenda kufanya nao kazi, kwa vile suala la mjusi ni suala mtambuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe upo hapa Mwenyezi Mungu akujaalie, mnafanya kazi vizuri Wenyeviti wa Bunge. Wabunge wangu Mwenyezi Mungu awajaalie awape afya njema ili twende tukafanye kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa umakini na ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa waliochukua mpira na kukimbia nawaende pembeni maana yake unaona, ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Ukiona wanalumbana ina maana wamefilisika hawana cha kufanya. Mheshimiwa Rais ambaye ni mtulivu, mwenye heshima yake na mwenye ujasiri wake, Mwenyezi Mungu amlinde aweze kufanya kazi na sisi tuko pamoja naye. Mwenyezi Mungu awalinde sana na aibariki Tanzania na Watanzania. Ahsanteni sana. (Makofi)