Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa fursa ya kuweza kuchangia na ninaomba niunge mkono hoja iliyopo mezani. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya upendeleo wa uzima na afya njema. Ni upendeleo kwa sababu wenzetu wengi walitamani kuiona siku ya leo lakini hawajaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara na shupavu, uongozi ambao umepelekea leo hii tuwe na matokeo makubwa lakini tuendelee kujivunia kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeeleza mambo mengi ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake wote ndani ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya. Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa sana ambayo kwa kweli kama Taifa tunajivunia: ujenzi wa miradi ya kimkakati; uhimilivu wa Deni la Taifa; mfumuko wa bei kuwa kwenye wigo ambao umewekwa; utoshelevu wa chakula nchini; amani na utulivu ambayo bado ipo; na uwekezaji katika Bandari yetu ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yamewezekana ili hali duniani kukiwa kuna misukosuko mikubwa. Kwa hiyo, ndiyo maana tunaendelea kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba uongozi wake ni imara, lakini pia uongozi wake ni shupavu sana japokuwa duniani kuna mambo yanaendelea wenzetu wanaporomoka, lakini sisi Tanzania tunaendelea kwenda viwango vya juu na kuwa kwenye ramani ya dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu uwekezaji wa bandari ulileta kelele nyingi sana na nikiwa kama Mbunge, Wabunge wa Dar es Salaam tuliungana kutoa elimu kwa Watanzania kwamba nini kinaenda kufanyika. Hakika tumeona kupitia taarifa ambazo zimeendelea kutolewa lakini kupitia uhalisia ambao tunaenda kuuona kama Wabunge tumetembelea mara kadhaa pale bandarini hakika mambo ni makubwa sana. Mheshimiwa Rais ni kiongozi ambaye hayumbi hatikisiki yuko imara na uimara wake tunauona umekuwa ukitoa matokeo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika penye ukweli uongo umeendelea kujitenga na mwaka huu ninaamini kabisa Watanzania wameendelea kuona na wataona na watafanya maamuzi sahihi kwamba ni kiongozi gani ambaye anafaa kuendelea kuiongoza Taifa letu, kwa sababu upotoshaji umekuwa ni mwingi na ni kwa sababu wenzetu wamekosa hoja. Hoja zote Mheshimiwa Rais amezikamilisha. Kwa hiyo, hawana cha kufanya, wanachokifanya ni kuendelea kupotosha kila iitwapo leo. Ninaamini kabisa niendelee kurudia kwamba Watanzania wana macho wanaona na watafanya maamuzi yaliyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niishukuru sana Serikali kwa huduma kwa watu wenye ulemavu. Tunaona kabisa kwamba Serikali imejipanga na ina mipango mingi kwa habari ya kundi hili la watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu. Mfuko huu ulianzishwa kwa Sheria Na.9 ya Mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu, kifungu cha 57(1) – (3), pale inaeleza ni kwa jinsi gani Mfuko unaanzishwa, malengo ya Mfuko huu, lakini pIa vyanzo vya fedha vya Mfuko huu wa Watu Wenye Ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya malengo ya Mfuko huu yalikuwa ni kutoa ruzuku kwa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu. Vilevile, kuendelea kufanya tafiti za masuala ya watu wenye ulemavu pamoja na kutoa huduma za utengamao na vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu. Fedha ambayo imeelezwa katika sheria hii chanzo kikubwa ni ile fedha ambayo inapitishwa na Bunge lako Tukufu, lakini pia fedha ambayo inapatikana kutoka kwa wadau mbalimbali na mambo mengine yako kwenye ile sheria ambayo yanajieleza vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, Serikali ina nia njema ya kuunganisha mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, lakini kwa kadri ambayo nimeeleza hapa na kwa jinsi ambavyo sheria inaeleza Mfuko huu malengo yake makubwa si uwezeshaji kiuchumi kwa watu wenye ulemavu ila ni kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu. Kama inavyofahamika ni kwamba kundi la watu wenye ulemavu bado lina uhitaji mkubwa hivyo niiombe Serikali Mfuko huu usiunganishwe na Mifuko mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa sababu malengo yake hayakuwa hayo ya uwezeshaji kiuchumi malengo yake ni kama ambavyo yanaelezwa kwenye sheria na kama ambavyo nimeyataja kwa uchache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu pia lilifanyia marekebisho Sheria ya Vyama vya Siasa. Niendelee kuiomba Serikali katika marekebisho yale kulikuwa na mkazo wa ujumuishi wa haya makundi maalum wakiwemo wanawake na watu wenye ulemavu, Serikali ifanye ufuatiliaji wa Sheria hii na hasa ikizingatiwa kwamba mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Ni kwa jinsi gani vyama vitakuwa vimetekeleza Sheria hii kwa kuweka ujumuishi wa makundi maalum na hasa kundi la watu wenye ulemavu. Tunatamani kuona watu wenye ulemavu wakishika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye vyama vya siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vyama hivi viweze kuona mfano mzuri ambao umewekwa na Chama Cha Mapinduzi wa kutenga nafasi maalum za watu wenye ulemavu kwenye nafasi hizi za Ubunge na kwenye level ya Madiwani. Vyama vione ni kwa jinsi gani kuanzia ngazi za Udiwani Viti Maalum pamoja na Kata kuweka nafasi zile za upendeleo kwa kundi la watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuishauri na kuiomba Serikali kipindi hiki ni kipindi cha uchaguzi iweze kuona ni kwa jinsi gani itaweka mbele matumizi ya lugha ya alama. Wenzetu viziwi ni wapigakura wazuri, lakini wanashindwa kuhudhuria hata kwenda kwenye mikutano kusikiliza sera za Wabunge, kusikiliza sera za madiwani kwa sababu kunakuwa hakuna ukalimani. Sasa tuweze kufikiria kwamba mtu anawezaji kupiga kura ambayo hajasikia sera zake. Hivyo niiombe Serikali iweke mkazo huu na ielekeze kwamba kuwe kuna matumizi ya lugha ya alama kipindi hiki cha uchaguzi, lakini wakati wote ili tuweze kuwa sambamba na wenzetu viziwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimekuwa nikiliomba kila mara Serikali iweze kuona ni kwa jinsi gani inaendelea kutenga fedha za ununuzi wa mafuta ya watu wenye ualbino na kuweza kuyasambaza na kuwafikia wahusika. Sambamba na hilo, tukiwa tunasubiri ule Mfumo mzuri wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali iweze kuona ni kwa jinsi gani inaweka uratibu mzuri na unaotekelezeka wa matibabu kwa watu wenye ulemavu wasiokuwa na uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya, ninaomba kushukuru na niunge mkono hoja tena. (Makofi)