Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaomba kuidhinishiwa bilioni 595.2 kwa shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini pia bilioni 186.8 kama Mfuko wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hotuba ya Waziri Mkuu imerejea utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kuzingatia utekelezaji wa dira ya mwaka 2025 inayoisha na pia ndio mwanzo wa utekelezaji wa dira nyingine ya miaka mingine 25. Ni kweli kwamba kupitia hotuba hii ya Waziri Mkuu Serikali imeonesha kwamba inaweza kusimamia kwa mambo ambayo imeyapanga na tunaona mafanikio makubwa sana kupitia utekelezaji wa dira inayokwisha. Ni katika msingi huo tunampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu mwenyewe kwa usimamizi mzuri, pamoja na Mawaziri wote ambao chini yao ndio wamekuwa wakisimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya miradi ambayo imeonesha kwamba Serikali inaweza ikasimamia vema malengo yake na moja ya miradi ambayo Watanzania wengi bila kujali jinsia zao, itikadi zao za kisiasa au kidini wamefurahia na wakaona kwamba inakata kiu yao wakati huu kwa wale ambao mradi huu umewafikia na kwamba ikajenga kiu zaidi kwa wale ambao mradi huu haujawafikia, ni Mradi wa SGR. Wale ambao tumefanikiwa kusafiri baina ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma kupitia SGR, tunaweza tukawa ni mashuhuda kwa jinsi ambavyo treni yetu imeweza kurahisisha usafiri kwa kuchukua abiria wengi kwa wakati mmoja. Kwa msingi huo kuondoa foleni barabarani ambayo wakati mmoja treni ikisafiri unahitaji mabasi 20 kufanya safari hiyo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeanza vizuri sana katika namna ambavyo SGR inaendeshwa. Mambo yafuatayo ninadhani ni ya msingi sana yakaendelea kusimamiwa vema. Jambo la kwanza ni ukataji tiketi kwa njia ya kidigitali. Tusingetamani kurudi nyuma kama ilivyokuwa kwa mwendokasi. Mwendokasi Dar es Salaam walianza kukatisha tiketi kwa kidigitali, lakini baada ya muda wakarejea nyuma na kuanza kukatisha kwa mkono. Tungetamani kwa jinsi ambavyo tumeanza vizuri na SGR mfumo huu wa ukataji tiketi kwa kidigitali uweze kuendelea kwa sababu unaona kabisa kwamba fedha inaingia moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi hiyo wataalam wa mifumo ya mtandao tunaomba wawe alert, wakae chonjo muda wote ili uendelee kufanya kazi kwa ufanisi siku zote. Tusije tukawa na cyber security attack ambayo inaweza ikaturudisha nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SGR ni treni ya umeme na kwa jinsi ambavyo Serikali imeanzisha mkoa wa SGR katika huduma ya nishati, basi wataalam wetu hawa wahakikishe sasa kwamba, katika huduma za SGR kusiwe na kile ambacho wakati fulani kilitokea cha kukatikakatika kwa umeme na hatimaye treni yetu ikasimama ghafla maporini mahali fulani. Kwa jinsi hiyo, iwapo wataendelea kudumisha huduma bora za kutoa huduma ya nishati katika SGR maana yake ni kwamba tutakuwa na huduma bora na huduma shindani ndani ya nchi yetu na kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usalama wa SGR; m. Mwanzoni tulipokuwa tunaanza tulishuhudia Watanzania wachache ambao walikuwa wanatamani kuhujumu miundombinu ya SGR. Hili jambo ni la msingi, uongozi uendelee kusimamia vizuri usalama ili kusiwe tena na watu ambao wanaweza wakahujumu miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, ninaomba niongelee kuhusu eneo la maegesho ya magari katika vituo vya Dodoma na Dar es Salaam. Pamoja na huduma nzuri inayotolewa, bado tunaona kwamba Dodoma kuna eneo dogo sana la maegesho ya magari; na si kwa sababu hakuna eneo la kutosha. Haya ni mambo ambayo tunadhani kwamba yanaweza yakaboresha ili kuondoa msongamano watu wanapokuwa wanashuka na hatimaye kuendelea kufurahia huduma za SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Serikali imeonesha inaweza kusimamia vema, basi vile vipande ambavyo vimebaki vya kuelekea Tabora, Mwanza pamoja na Kigoma, basi Serikali katika hatua inayofuata ya utekelezaji wa bajeti ifanye lile linalowezekana ili vipande hivi navyo viweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nitaliongelea ni kuhusu ushindani wa kibiashara unaoendelea duniani kati ya mataifa makubwa yenye uchumi mkubwa. Sisi kama Taifa ambalo bado linaendelea kupiga hatua, hatuwezi tukakaa na tukatazama bila kutafuta nafasi yetu katika mtanzuko huu unaoendelea. Tumeshuhudia mataifa makubwa mawili ambayo kila kunapokucha mwingine anaongeza kodi juu ya vile vinavyoingia nchini kwake na mwingine pia anaongeza. Jambo hili linaweza likaathiri mataifa ambayo yanaendelea na sisi hatuwezi tukakaa kimya. Hivyo, ni jukumu la Serikali kila wakati kuangalia mwenendo wa biashara unavyoendelea katika mataifa haya ili sisi tuone kwamba tunajiweka mahali gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ni la msingi katika hili ni kwamba, kama Taifa litajitosheleza kwenye chakula kwa maana ya kwamba tukawa na usalama wa chakula ndani ya nchi, basi Taifa ambalo limeshiba linaweza likawa linaendelea na mienendo katika mataifa mengine, lakini tukiwa tuna hakika ya kwamba, sisi tuna akiba ya kutosha ya chakula ndani ya nchi na pia tuna ziada ambayo pia tunaweza tukauza nje ya mipaka yetu na hasa katika Soko la Afrika Mashariki na SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunadhani kwamba lazima tuuze nje mbali, lakini yawezekana kabisa kwamba ndani ya SADC pamoja na Afrika Mashariki bado kuna soko linalohitajika kwa ajili ya kuuza chakula. Kwa jinsi hiyo, Wizara ya Kilimo iendelee kukifanya kilimo kiweze kuwa cha kuvutia hasa kwa vijana wa Taifa hili ili kuongeza tija, ajira lakini pia wakati huohuo kuwaondoa katika mambo ambayo yanawapotezea muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kilimo kikiwa cha kuvutia hakuna sababu ya vijana wetu kwenda kufanya betting. Wanapotelea huko kwenye betting wakidhani kwamba wanatengeneza faida kumbe kama kilimo kingekuwa cha kuvutia kikatengeneza faida hakuna sababu ya kupoteza fedha katika betting. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Serikali isimamie sana uwiano wa kibiashara ili kwamba tuzalishe sana mashambani, migodini, viwandani, katika misitu, uvuvi pamoja na ufugaji; ili kwamba tukifanya uwiano wetu wa kibiashara ukawa mzuri ndani ya nchi lakini katika jumuiya inayotuzunguka. Kile nilichokiongelea cha kwamba kuna ushindani wa kibiashara unaoanza kutokea baina ya mataifa makubwa ya kiuchumi hakutaweza kutuathiri kwa kiasi kikubwa na hivyo Serikali iweze kukaa chonjo muda wote ikiendelea kufanya tathmini ya jinsi ambavyo hatua zinazochukuliwa nje yetu haziwezi zikatuathiri hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo ninakushukuru na ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)