Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa maandalizi mazuri na hotuba ndefu ya saa mbili ambayo tuliisikia hapa wiki iliyopita. Nipende kusema kwamba, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kwa kirefu sana mafanikio makubwa ambayo nchi yetu imeyapata katika kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa madarakani; ni mafanikio makubwa na sisi watu wa Njombe kama Mkoa hususan Jimbo la Njombe Mjini ni mashuhuda wa mafanikio makubwa hayo ya kuwasogezea wananchi wa Tanzania huduma mbalimbali za kuboresha miundombinu kama vile madarasa, usafiri wa reli, usafiri wa anga na mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa haya yote ambayo yamefanyika. Sisi Njombe tunasema tumefanyiwa mengi katika kipindi hiki kifupi. Siwezi kuyataja yote, lakini nitataja yale ambayo ni machache ambayo yalikuwa ni makubwa na kero kubwa ambazo zimefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa ya Mji wa Njombe ilikuwa ni maji; hatukuwahi kuwa na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya maji; lakini kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka minne tumekuwa na miradi mikubwa minne ya maji. Miradi mwili kati ya hiyo minne imekwishakamilika na imekwishaanza kuleta maji katika Mji wa Njombe. Vilevile, tunavyoongea kwa mara ya kwanza kwa wananchi wa Njombe ambao wana maji mengi ambayo Mungu amewajalia, bado walikuwa katika mgao wa maji safi na salama. Kwa mara ya kwanza kwenye kiangazi hiki wameanza kuonja matunda ya uwekezaji huo mkubwa wa miradi mikubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mradi wa Ijunilo bilioni 3.9; tuna Mradi wa Livingstone bilioni 9.8; tuna Mradi wa Miji 28 ambao unakwenda kwa kasi, bilioni 41. Kwa hiyo, jumla tuna bilioni kama 67 katika maji peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme, vijiji vyote sasa hivi vina umeme na sasa tunakwenda kwenye vitongoji. Hata hivyo, ni angalizo kidogo; Mji wa Njombe ni Mji na vijiji. Bado kuna maeneo ya mjini baadhi ya mitaa hakuna umeme na wananchi wa Njombe wananisikia. Maeneo kama ya Mpumbwe pamoja na Ihanga yote hayo bado yana tatizo la umeme. Nina hakika katika mpango unaokuja ingawaje si vitongoji na ni mitaa nayo yataangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya yamefanyika mambo makubwa sana. Ndani ya Mji wa Njombe tuna Hospitali kubwa ya Rufaa ya Mkoa ambayo Serikali imeingiza pale bilioni 27.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hospitali ambayo imebadilisha maisha ya Wananjombe. Uwekezaji huu ni mkubwa, capacity ya vitanda ni 400, lakini vitanda vilivyopo mpaka sasa ni 238. Mama na Mtoto peke yake ni vitanda 100 na akinamama 12 wanaweza wakajifungua kwa wakati mmoja. Ni mambo makubwa ambayo yamefanyika katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi, ipo pia kampasi ya Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo inakuja Njombe yenye thamani ya bilioni 18. Tuna kiwanja cha ndege, tumesikia nacho kinakuja kwa kasi Njombe; kwa maana ya kwamba Serikali imeridhia na tunaanza kutafuta eneo. Tunawashukuru wenzetu wa Serikali ya mkoa ambao wanalishughulikia suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo letu ambalo ninapenda nitoe ushauri ni kwenye uwekezaji, ambalo ndilo eneo kubwa, na ninamshukuru Profesa Muhongo ameniwekea msingi wa hoja yangu. Shida yetu sisi ni kutengeneza ajira katika Mkoa au Mji wa Njombe. Njombe kwa kiasi kikubwa inategemea kilimo, kwa 99%. Kilimo chetu sisi ni kilimo cha mazao ya chakula na mazao ya biashara. Vilevile, tunategemea mazao ya misitu. Hapa ndipo ambapo kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, amekuja Njombe takribani mara mbili na mara zote amejaribu sana kushughulikia changamoto zinazohusiana na uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa nipende kusema, sekta ya uwekezaji wa chai ndio uwekezaji mkubwa sana kwa Njombe kwa miaka mingi sana. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2018 sekta hii imedorora. Tunafahamu jitihada za Serikali kutaka kufufua au kuhakikisha kwamba sekta ya chai inafanya kazi vizuri. Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba kuna kukosekana kwa umakini katika kutafuta wawekezaji. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake, katika kipindi hiki imetengeneza mazingira mazuri sana ya wawekezaji wa ndani na wawekezaji wa nje; na tumeona mabadiliko mengi ya Sheria ya kutaka kuvutia uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani inabidi tufanye tahadhari. Tuna wawekezaji wa aina nyingi wanaokuja kwa mwamvuli wa uwekezaji. Kwa kiasi kikubwa tusipokuwa makini, hasa na wawekezaji wanaokwenda vijijini na kujifanya wao wana uwezo mkubwa wa kusaidia kilimo, lakini mwisho wa siku tunachokiona ni kwamba wananchi ambao wanategemea kilimo, kwa maana ya kuwategemea wawekezaji ambao wanajenga au wananunua viwanda, na hasa ninaongelea viwanda vya chai, wamekuwa ndicho kiini cha kusogeza umasikini na kupunguza au kuondoa ajira kwenye maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lazima tulipige vita kama nchi. Kwa sababu tunahitaji ajira, tunahitaji kodi na tunahitaji mazao ya kupeleka nje ili tupate fedha za kigeni. Tunapompa mwekezaji kama wa chai; na nitakuwa more specific, kwa mfano tuna uwekezaji wa chai wa kampuni inaitwa DL ambayo imekuwa mwiba mkubwa sana kwa wananchi wa Njombe; pamoja na jitihada, ninachopenda kusema ni kwamba, Serikali iwe tayari kufanya maamuzi magumu kwa wawekezaji wa aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji kwenye eneo la chai wanapewaa ardhi. Ardhi ni productive asset. Kama haitumiki kuzalisha ajira, kuzalisha bidhaa, haitumiki kuleta fedha za kigeni maana yake ni kwamba hatuitumii ardhi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuondoa na kustawisha maisha ya wananchi wetu. Kwa hiyo, mwekezaji ambaye anahodhi ardhi na hafanyii kazi, niombe sana kwamba; Ofisi ya Waziri Mkuu inafanya uratibu, na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja Njombe zaidi ya mara moja; tuwe na mkakati wa Kufanya maamuzi magumu, ikiwezekana kuichukua hiyo ardhi. Sisi ni wananchi wa Tanzania na Mwenyezi Mungu ametupatia ardhi, ni lazima itumike kwa watu ambao wako tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine ambalo liko kwenye misitu, nako ni suala kubwa la ajira. Ninapenda kusema, tuna kampuni kubwa pale ya Kibena (TANWAT) huo ndio mfano halisi wa kampuni ya uwekezaji ambazo tunataka uje kwenye maeneo kama ya Njombe na maeneo mengine ya Tanzania. Ni kampuni ambayo inazalisha ajira, inafanya plantation za mazao mbalimbali na ikipewa ardhi inaitumia. Vilevile, kwa siku za hivi karibuni, tumeanza kuona kampuni nyingine nyingi ambazo zinatoka pande za Asia zikija kwa jina la kutaka kuwekeza kwenye upande wa sekta za misitu. Uhalisia ni kwamba kampuni hizi zinakuja kufilisi nchi, kwa maana ya wananchi wa maeneo yanayozunguka. Hawa kazi yao ni kupata mazao ya mbao na kuyasafirisha yakiwa ghafi au semi-processed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hiyo process nchi inapoteza ajira, nchi inarudi kwenye umasikini, kwa maana ya wananchi waliopo kwenye yale maeneo badala ya kupanda miti kwa wingi wanaendelea kufyeka miti na kuzipelekea kampuni hizo za Kichina, ambazo kwa kweli tunasema ni uwekezaji ambao hauna tija kwa sababu hawana jukumu la kuzalisha miti, kupanda miti, wao ni kupokea mazao ya miti ambayo hawajui yanatokea wapi, wanawalipa wananchi fedha ndogo kwa sababu wananchi wetu wana shida na hizo fedha. Sasa, Serikali ina jukumu la kuhakikisha kwamba inawalinda wananchi wake na kuhakikisha wawekezaji kama hawa hawapewi vibali vya kuja kukata miti hovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwamba, jambo hili tumeliongea hapa na wameanza kuchukua hatua. Tunafahamu wana kitu wanakiita Mpango Mkakati wa Mwaka 2021 mpaka 2030 wa kuangalia namna gani tunaongeza thamani kwenye mazao ya misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huo bado kuna GN ya 2023 (GN. 211) ambayo bado inaruhusu au inaratibu usafirishaji wa malighafi za misitu kwenda nje. Ndani ya GN hiyo tuna mategemeo na tumepiga kelele sana hapa, tunaitaka Serikali kwa kweli ihakikishe kwamba inatumia GN hiyo kuzuia kutoa vibali kwa wawekezaji wa aina hii ambayo nimeitaja, ambao mpaka muda huu wanafanya na wamehalalishwa na Wizara yetu ya Maliasili kuendelea kukata miti na kuwafanya wananchi wasiweze kufaidi matunda ya miti hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mategemeo yangu; tuliambiwa hapa kuwa vibali hivyo wamepewa kwa mara ya mwisho. Hata hivyo, mwaka juzi tuliambiwa hivyo hivyo kuwa wamepewa kwa mara ya mwisho. Ni matumaini ya watu wa Njombe kwamba kama hakutakuwa na improvement au kuwataka waongeze thamani na ajira ndani ya nchi ni bora tuhakikishe vibali hivyo havitolewi tena kwa kwa wawekezaji wanaotoka maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, niongelee kwa kifupi kuhusu Liganga na Mchuchuma. Sisi tunaishukuru sana Serikali, kwa mara ya kwanza tumepewa taarifa hapa ndani ya Bunge lako kwamba sasa nchi yetu imepiga hatua nyingine katika kuhakikisha kuwa uwekezaji kwenye Liganga na Mchuchuma unakwenda kwenye hatua nyingine. Tunaishukuru sana Serikali na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake binafsi za kuhakikisha anafufua uwekezaji huo na sasa tunangojea majadiliano ya mwisho ambayo tunasikia yanafanyika wiki ijayo ili tuweze kupata uwekezaji mkubwa wa Liganga na Mchuchuma katika Mkoa wa Njombe. Ninakushukuru sana.