Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango wangu kuhusu Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nadhani tuipitishe hii bajeti kusudi Waziri Mkuu na timu yake waendelee na kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa sehemu mbili, nitaongelea kwenye sera na kwenye ajira. Hii bajeti ni muhimu kwa sababu, inamalizia Dira yetu ya 2025 na inaanza utekelezaji wa Dira yetu ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sera nitaongelea Sera ya Maafa ambayo inahitaji marekebisho makubwa, lakini kabla sijaenda mbali naomba niendelee kutoa pole nyingi sana kwa ndugu zangu wa Musoma Vijijini ambao tumepatwa maafa ya nyumba 84 ambazo zimebomoka na wale jirani zetu wa Musoma Mjini vilevile walipata maafa makubwa. Poleni sana na tunashukuru Serikali imeanza kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Maafa inapaswa kuboreshwa kwa sababu zifuatazo. Sababu ya kwanza ni sera yetu tuliyonayo haiendani na hali halisi kwa sababu, maafa yamekuwa mengi na ni ya aina tofautitofauti. Kwa mfano, kwa sasa tuna maafa yanayotokana na madhara ya tabianchi, haya ndiyo kama ukame, moto, mafuriko, dhoruba huko ziwani na baharini na tuna maafa mengine yanayotokana na, tuseme hayakupangwa hayo ni natural, kama tetemeko la ardhi au milipuko ya volkano. Kuna maafa ambayo yanasababishwa na vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa hiyo, ni lazima sera yetu tuipitie upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni kwamba, Watanzania wameongezeka wamekuwa wengi kwa hiyo, maafa yakitokea hayaendani na hali halisi ya kukabiliana nayo. Mwaka 1961 wakati tunapata uhuru tulikuwa Watanzania karibu milioni 10, sasa hivi tukifika mwishoni mwaka huu tutakuwa tumevuka watu milioni 70 na dira ya maendeleo yetu ya Mwaka 2050 tukifika Mwaka 2050 tutakuwa Watanzania milioni 137. Kwa hiyo, inabidi tuboreshe sera hii ya maafa na uboreshaji wake cha muhimu ni lazima iendane na upatikanaji wa vyanzo vya fedha za kukabiliana na maafa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uzoefu wa dunia nyingine, maafa madogomadogo huwa yanashughulikiwa na local government, Serikali ya Mitaa. Kwa kule Marekani yanashughulikiwa na majimbo na hata kule China vilevile yanashughulikiwa na Serikali za Majimbo, kwa hapa kwetu ni kama vile halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maafa makubwa sana yanashughulikiwa na Serikali Kuu (Central Government), ndiyo maana kule Marekani unasikia Federal Government imeingilia kati na yanashughulikiwa na taasisi na NGOs za kimataifa, kama Red Cross, halafu ushirikiano wa nchi kwa nchi. Chanzo cha tatu cha fedha za maafa ni zinatokana na bima; sasa sisi hatuna bima nyingi ndiyo maana maafa yanashindwa kuhudumiwa. Kwa hiyo, tukishaipitisha hii bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, napendekeza sana tupitie sera yetu ya maafa iendane na vyanzo vya maafa halafu iendane na upatikanaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili ninachokiongelea ni ajira. Ajira vilevile naiangalia, tunamaliza Bajeti ya Dira ya Mwaka 2025 tunataka ajira inayotupeleka kwenye Dira ya mwaka 2050. Sifa kuu za ajira ni mbili, elimu na cha pili ni mafunzo na nguzo ya ajira zote ni uchumi. Kwa hiyo, ajira zitategemea uchumi wa sekta binafsi, ajira zitategemea uchumi wa Serikali nzima na taasisi zake. Kwa mataifa yote duniani kote mwajiri mkubwa huwa ni sekta binafsi na siyo Serikali kwa hiyo, ajira ninazoziongelea mimi ni za miaka 25 inayokuja kufika mwaka 2050. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Tanzania, ajira tuzitoe kwanza sekta binafsi ndani ya Tanzania na sekta binafsi nje ya Tanzania. Pili, ajira tuzitoe kwenye Serikali ya Tanzania na zitoke kwenye Serikali za Mabara mengine, yaani huko Ulaya, Marekani, Asia na nchi za kiafrika. Watu wanaweza kuajiriwa na Serikali za huko na siyo lazima kutegemea Serikali ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mahitaji makubwa ya hizi ajira, wanataka sana mambo ya sayansi, teknolojia na innovation. Nina mifano hapa, mitatu minne, nitakayoitoa ambayo ajira zina soko kubwa huko kwenye dunia nyingine, upande wa afya, upande wa teknolojia, artificial intelligence, hiki siyo kitu kipya; mara ya kwanza, semina ya kwanza ya artificial intelligence ilifanyika Marekani mwaka 1956 siyo kitu kipya, halafu na mambo ya manufacturing, uzalishaji viwandani. Hayo maeneo manne yatawapatia vijana wetu kazi nje ya Tanzania kama tutakuwa tumejipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hii artificial intelligence ni kubwa mno, ni kufanya kazi kama mashine na wanataka data scientists na ndugu zangu data centres ndiyo zinachukua umeme kuzidi hata viwanda vikubwa. Sasa hivi duniani kwa siku tunatumia umeme karibu trilioni 70 za watts na asilimia mbili ya huo umeme inaenda kwenye data centres. Kwa hiyo, ndiyo maana watu wengi wanatakiwa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, umuhimu wa kazi za nje ni vijana wetu kupata kazi huko nje halafu na pato la kitaifa kuongezeka, sasa hizi kazi za nje imekuwa ni biashara, ni bidhaa mpya duniani. Kwa mfano, mwaka 2023 bidhaa hii ya kazi za nje na watu kupeleka fedha nchini kwao ilikuwa na thamani ya dola bilioni 867 na mwaka jana hii bidhaa ilikuwa na thamani ya dola bilioni 905. Ndani ya mwaka mmoja tu zimeongezeka asilimia 4.6 za bidhaa hii. Hakuna biashara yoyote utakayoweza kuipata ndani ya mwaka mmoja inaongezeka kiasi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana, ili kuona umuhimu wa sisi kutafuta hizo kazi za nje, waliopata pesa nyingi, kipato kingi, remittances na kurudisha kwao fedha, ya kwanza ilikuwa India. India ilirudisha fedha shilingi bilioni 129, inashinda kuuza pamba yetu nje. Mexico ilikuwa ya pili, shilingi bilioni 66, China ilikuwa ya tatu shilingi bilioni 50. Kwa hiyo, kwa upande wa Bara la Afrika tukichukua tano bora, ya kwanza ilikuwa Egypt kazi za nje hizo, ilitengeneza shilingi bilioni 30, ya pili ilikuwa Nigeria shilingi bilioni 21, ya tatu ilikuwa Morocco shilingi bilioni 12, nusu dakika, namalizia; kwanza sikuwepo, niongezee muda kidogo. Halafu Morocco shilingi bilioni 12, Ghana shilingi bilioni 7.0 na Kenya shilingi bilioni 5.0. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba, kama tunataka ajira zipo nje. Jambo la muhimu ni elimu na mafunzo na nimalizie hapa kwenye mafunzo, lazima tuwekeze kwenye sayansi, teknolojia na innovation, yaani kwa lugha nyingine hayo masomo yanaitwa STEM (Science, Technology, Engineering and Mathematics) kuanzia shule zetu za awali na shahada za vyuo vyetu vikuu ziwe shahada zinazotakiwa huko dunia nyingine. Ahsante. (Makofi)